Header Ads

FUNDI Pancha Atupwa Jela Miaka 30 Kwa Kukutwa na Misokoto 601 ya Bangi

Fundi wa kuziba pancha, Harson Solomon (38), mkazi wa wilayani hapa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kupatikana na misokoto 601 ya bangi.

Kifungo hicho kimeangukia sheria mpya ya udhibiti wa dawa za kulevya iliyosainiwa Mei 11, 2015 na aliyekuwa Rais wakati huo, Jakaya Kikwete. Imeelezwa Solomon ni miongoni mwa washtakiwa wa mwanzo kufungwa kwa sheria hiyo.

Awali, sheria ilikuwa inatoa mwanya wa faini na mtu anaposhindwa kulipa ndipo hutumikia kifungo jela lakini hivi sasa anayepatikana na hatia ya kukutwa na kiwango kikubwa hutupwa jela.

Kifungu cha 11(1) D cha sheria hiyo mpya, kinaeleza wazi mtu anayezalisha, kumiliki, kuuza, kununua au kusafirisha dawa za kulevya ikiwamo bangi, adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 30 jela.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Joachim Tiganga baada ya kuridhishwa bila kuacha shaka na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka alidai kortini kuwa Desemba 1, 2015 katika maeneo ya Mwika Kimangara, Moshi Vijijini mshitakiwa alipatikana na kiasi hicho cha bangi.

 Pia, anadaiwa kuruhusu eneo lake kutumika kuuza bangi na gongo.

Akisoma hukumu, Hakimu Tiganga alisema matumizi ya dawa za kulevya yanazidi kuongezeka nchini na kuathiri jamii, hivyo Mahakama inatoa adhabu hiyo iwe fundisho kwa wengine.

Katika kipindi chote tangu afikishwe kortini kwa mara ya kwanza Desemba 11 mwaka jana, mshtakiwa alikana mashtaka hadi alipotiwa hatiani na kuhukumiwa jana.

No comments

Powered by Blogger.