Header Ads

WASANII KUTEKETEA KWA KUBWIA MADAWA YA KULEVYA, JE NINI TATIZO? TUPATIE MAONI YAKO

NI mtihani. Ndivyo unaweza kusema, hasa baada ya kundi kubwa la vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 30 kujikuta likiteketea kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Kutokana na hali hiyo, kundi la wasanii wa muziki wa kizazi kipya na vijana wa kimaskini wamekuwa ni waathirika wakubwa hali inayotishia nguvu kazi ya Taifa.

Kundi la hilo la wasanii sasa limegeuka mateka, huku hali hiyo ikichangiwa na wafanyabiashara wakubwa nchini, ambao wamekuwa wakiwashawishi kwa fedha na hata kuwahonga magari ili waweze kutumia mihadarati.

MTANZANIA ilizungumza na baadhi ya wasanii ambao sasa wamejikuta katika matumizi ya mihadarati hiyo na hata kuonekana kuwaumiza huku wengine wakiwa kama wendawazimu.

Mmoja wa wasanii wa muziki wa kizazi kipya, Abubakari Katwila, maarufu Q-Chief, ambaye anatajwa katika matumizi ya dawa za kulevya, alisema kwa sasa ameacha baada ya kukubali kuwa alipotea.

Alisema wakati anaingia katika matumizi hayo ya mihadarati hakushawishiwa na mtu, bali alijikuta ametumbukia katika hali hiyo.

“Nilikuwa muathirika wa dawa za kulevya, nimejitambua nimeacha mimi mwenyewe bila kulazimishwa na mtu, huwezi kumtibu mtu ambaye hajajikubali hili ni tatizo,” alisema.

FEROOZ
Ferooz Mrisho ambaye katika miaka ya 2000 alitamba na wimbo wa Starehe ambao ulikuwa ukihamasisha mapambano dhidi ya Ukimwi, ambaye kwa sasa ameathirika na dawa hizo, alisema inamuwia vigumu kuachana na matumizi ya dawa hizo.

Alisema pamoja na hali hiyo, amejikuta akitenga bajeti kubwa ya fedha kwa matumizi ya kutumia dawa, ingawa alipoulizwa ni wapi anaponunua hakuwa tayari kutaja.

“Ninawaomba wasanii wenzangu wasitumie dawa maana ni vigumu kuacha.  Natamani sana kurudi kama zamani ili heshima yangu iwepo ila inanisumbua, lakini naamini iko siku,” alisema Ferooz.

Wasanii wengine ambao wanahusishwa na tuhuma za matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na Geez Mabovu, Daz Baba, T.I.D, Ray C, Lord Eyez, Rashidi Makwilo ‘Chid Benz’, 20%, Terry Fanani,  Sister P, Msafiri Diouf, Rachael Kiuno, Mandojo, Domokaya, Rose Mhando na Nando ambaye hivi karibuni alishiriki mashindano ya Big Brother (BBA).

Mmoja wa wasanii hao ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazeti, alisema kuwa pamoja naye kujikuta anatumia dawa za kulevya, lakini bado Serikali inajua watu wanaoingiza dawa hizo na wameshindwa kuwachukulia hatua.

“Kula dawa inahitaji gharama, maana inafika mahali ili niweze kupata kete walau moja kila siku asubuhi inanibidi nitafute Sh 3,000. Lakini pia hufika mahali natumia hadi Sh 15,000 kwa siku.

“Wapi napata pesa? Unajua licha ya hii kazi yangu ila bado kuna jamaa zangu wanene (wafanyabiashara) ambao nao hutumia, ukiwapigia simu hukosi 20,000 au hata 100,000. Na mimi nilipoingia katika matumizi haya jamaa yangu mmoja alinishawishi kuwa nikitumia hii atanipa safari, kumbe nilikuwa naonja ili kujua ubora, basi hadi leo nimejikuta natumia,” alisema msanii huyo.

Matumizi ya dawa za kulevya yanatajwa kusababisha vifo vya wasanii kadhaa wakiwamo Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’, Aisha Mohamed ‘Aisha Madinda’,  Albert Mangwea ‘Ngwea’, Langa, Grace Mbawala na Esther Bondia.

Licha ya hilo, taarifa za ndani zinaeleza kuwa aliyekuwa msanii nyota wa Bongo Movie, marehemu Steven Kanumba pia anahusishwa na matumizi ya dawa hizo.

Inalezwa kuwa baada ya kifo chake, alikutwa katika kucha akiwa na chembe za unga unaosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya, ambazo baada ya kutumia alikunywa pombe kabla ya kuingia katika ugomvi unaodaiwa kusababisha mauti yake.

VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, vita dhidi ya matumizi ya dawa hizo imeendelea kupata changamoto nyingi kutokana na kukithiri kwa uingizaji wake.

Tume hiyo ilidai kuwa kiwango cha dawa zinazoingia na kukamatwa kimepanda kutoka kilo tatu za dawa aina ya Heroin mwaka 2008 hadi kilo 265.54 mwaka 2011 na kilo nne za dawa aina ya cocaine hadi kufikia kilo 128.30 kwa mwaka huo.

MSAKO WA WASANII WABWIA UNGA
Akizungumza na MTANZANIA, Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Mihayo Msikhela, alisema hivi sasa wapo kwenye msako dhidi ya wasanii ambao wamekuwa wakisambaza ujumbe wa matumizi ya mihadarati hiyo.

Alisema wasanii hao ambao ndio kioo cha jamii, sasa wamekuwa wa kwanza katika kusambaza ujumbe wa matumizi hayo.

“Mimi binafsi simfahamu Chid Benz kama ni mtu maarufu aliyekuwa akifahamika kwa kiasi hicho, lakini baada ya kumuona kwenye mitandao ya kijamii ndipo nikaanza kumfuatilia,” alisema Kamishna Msikhela.

Alisema endapo wakipata taarifa ya kwamba wanatumia hadharani na kuwakamata, basi watachukuliwa hatua kama wahalifu wengine.

“Hawa wasanii tunawasaka nao watuhumiwe kama wahalifu wengine na wakichukuliwa hatua itakuwa fundisho kubwa kwa vijana ambao walikuwa na nia ya kujiingiza katika mtandao huo,’’ alisema.

Alisema ni vema kwa vijana wasiwafuate watu maarufu ambao kwa namna moja ama nyingine wanaushawishi mkubwa kiasi  katika matumizi ya dawa hizo.

Kamishna Msikhela alisema wimbi kubwa la vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 30 ndilo ambalo linajiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya jambo ambalo ni hatari kwa Taifa.

“Vijana hawa ndio ambao wangekuwa tegemeo, vijana wa umri huo ndio ambao wangekuja kuwa viongozi wa baadaye, yaani kwa umri huo ndiyo wanaandaliwa kuwa madereva, mawaziri, wakulima, lakini leo wanakuwa mateja, ni jambo la hatari sana,’’ alisema.

MIKAKATI
Kamishna Msikhela alisema Jeshi la Polisi kwa sasa liko katika mkakati maalumu wa kuhakikisha elimu katika jamii inatolewa ili wananchi waweze kuelimika.

Alisema ulimaji wa bangi mashambani ni mkubwa kuliko mirungi, lakini aliongeza kuwa kama mateja mitaani wanapungua basi hata uingizaji wa dawa hizo kwa sasa nao umepungua.

KAULI YA WAZIRI
Juzi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alisema wimbi la magenge, wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya wameongezeka kwa kasi.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa kwa wale wanaojihusisha kwa namna yoyote ile ni vyema wakaamua kuachana nayo kabla hawajakumbwa na mkono wa dola.

Alitoa kauli hiyo baada ya kufanya mazungumzo na mama mzazi wa msanii Chid Benz, ambaye amepatwa na tatizo la matumizi ya dawa za kulevya.

“Inasikitisha na haivumiliki kuona nguvu kazi ya Taifa inapotea huku wauzaji wakinufaika kwa pesa haramu, ifahamike wazi vita ya Serikali dhidi ya wauzaji ni kubwa kuliko wanavyofikiria,” alisema.

VIONGOZI WA DINI
Wakizungumza na MTANZANIA, viongozi mbalimbali wa dini walisema kuwa ipo haja kwa jamii na Serikali kuwa na hofu ya Mungu.

Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Bukoba, Dk. Method Kilaini, alisema kama viongozi wa dini inabidi watoe elimu ya dini kwa nguvu zote na kuwaweka vijana wawe na hofu ya Mungu.

“Elimu ya kumweka kijana katika maombi awe karibu na Mungu hili litasaidia sana kujitoa katika mtego huo wa shetani na si vinginevyo,” alisema Askofu Kilaini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata),  Sheikh Hamis Mataka, alisema Serikali haitakiwi kumwacha mtumiaji wa kawaida kwani naye ni muhalifu pia.

Alisema vita hivyo ni vema vikafanyika kwa kuangalia kila eneo badala ya sasa kupambana na waingizaji, huku watumiaji wakiachwa kwani suala hilo haliwezi kumalizika.

“Kwa upande wa dini tunatakiwa kuanza kuwaelimisha watoto wetu juu ya dhambi hii huko kwenye madrasa sio kufundisha Kuran tu, wazazi sasa hivi wanalea kidigitali, hivyo mtoto kufanya dhambi anaona ni kitu cha kawaida.

“Tuanze kuwaonyesha watoto wetu namna ya kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, hii naona itapunguza, pili hata hao vijana walioathrika wasipelekwe tu ‘Sober House’ kwa sababu ya matibabu, pia wapate nasaha kutoka kwa viongozi wa dini ili wakibadilika wabadilike kiuhakika,’’ alisema Sheikh Mataka.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili inayoshirikisha viongozi wa dini, Askofu William Mwamlanga, alisema Taifa linahitaji maombi mazito kwani Serikali imeshindwa kudhibiti hali hiyo na vijana wanaendelea kuangamia.

“Pia kesho (leo) tuna kikao cha wajumbe wa dini zote ambao mimi ni mwenyekiti wao, tutajadili hali hii kwani tulikubaliana sekta za dini zisiwe chaka la kubebea dawa hizo haramu ambazo pia ni katazo la Mungu,” alisema Askofu Mwamalanga.

VIONGOZI WA WASANII
Akizungumzia hali hiyo, Rais wa Shirikisho la Wasanii wa Filamu Tanzania (TAFF),  Simon Mwakifamba, alisema dawa za kulevya ni janga la Taifa.

Alisema ni vyema kila mmoja anapoona mwenzake ameathirika afikirie kwa makini kuwa na yeye kesho anaweza kufika hapo alipo mwenzie.

Rais wa Shirikisho la Madansa, Super Nyamwela, alisema baada ya kifo cha wasanii wenzao, akiwamo Aisha Madinda, walichukua tahadhari kubwa ikiwamo kufanya utafiti na kubaini kuwa wengi waliotumbukia katika matumizi hayo walitumia sigara wakiwa kazini.

WALIONASULIWA WAKAKWAMA
Mara kadhaa viongozi wa kitaifa wamekuwa wakichukua juhudi mbalimbali ikiwamo kuwasaidia wasanii hao, akiwamo mwanamuziki Rehema Chalamila ‘Ray C’ ambaye alisaidiwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwa kuhakikisha analipia matibabu yake ili aweze kuachana na dawa za kulevya.

Mbali na huyo pia Chid Benz alisaidiwa na Meneja wa Dimond, Babu Tale kwa kumpelea Sober House mjini Bagamoyo ambako alifanikiwa kuacha na baada ya muda alirudia tena kutumia mihadarati hiyo.

Source: Mtanzania

No comments

Powered by Blogger.