Header Ads

POLISI kufukua kaburi la binti aliyezikwa kwa siri Arusha

Familia moja  jijini Arusha inadaiwa kumzika kwa siri mtoto wao mdogo wa kike wa miaka mitatu katika kaburi lililofichwa, huku majirani wakidanganywa kuwa binti huyo yupo hai.


Taarifa za kisa hicho cha kusikitisha zimevifikia vyombo vya usalama. Kwa sasa kuna mipango ya kuhakikisha kuwa mwili wa binti huyo, Nuru Losipha aliyezikwa kwa siri na familia yake, unafukuliwa kwa uchunguzi zaidi.


Inadaiwa kuwa Losipha alipoteza maisha wakati akifanyiwa tohara au ukeketaji na ngariba, ambaye jina lake halikufahamika mara moja, huku familia yake ikishuhudia.


Kitendo hicho kilifanyika katika kijiji cha Engutoto Kata ya Mwandeti wilayani Arumeru Desemba 28, mwaka jana, zikiwa zimebaki takriban siku tatu tu, kabla ya mtoto huyo aliyekuwa na umri wa miaka mitatu tu, hajaingia mwaka mpya wa 2017.


Mtendaji wa Kata ya Mwandeti, Njivaini Kivuyo awali alikuwa amepitwa na taarifa hizo hadi vyombo vya habari vilipotinga kijijini hapo kwa uchunguzi na ndipo alipolazimika kwenda kuripoti tukio hilo kwenye kituo cha Polisi cha Ngaramtoni.


Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo aliapa kuwa liwalo na liwe na kwamba ikiwezekana kaburi litafukuliwa ili mwili wa malaika huyo asiye na hatia, uchunguzwe upya.


“Ndio kwanza nazipata hizi taarifa, na kama polisi tutaomba kibali cha mahakama ili twende kulifukua kaburi husika tujiridhishe kama kweli mtoto huyo amezikwa humo na iwapo tutaukuta huo mwili, basi tutaanza uchunguzi juu ya kifo chake,” alisema Kamanda arles Mkumbo.


Baba wa marehemu, Losipha Kaiser anadai kuwa mtoto wake alifariki kutokana na ugonjwa wa baridi yabisi na kwamba aliugua kwa kipindi kirefu kabla ya kupoteza maisha Desemba 28, mwaka jana. Lakini madai yake hayo yanapingana na ripoti ya muuguzi katika duka la dawa lililopo kijiji cha jirani cha Kidali, anayeitwa Jane Andrew.


“Walimleta mtoto hapa walitaka nimsaidie tiba, lakini tayari huyo binti alikuwa amezimia na kutokwa na damu nyingi,”alidai.


Muuguzi huyo aliwahimiza wamkimbize mtoto hospitali, na hakufahamu nini kiliendelea hadi ripoti za kifo zilipomfikia.


Huku serikali ikipiga marufuku vitendo vya ukeketaji kwa wasichana, bado kuna familia nyingi kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa, zinaendeleza mila hiyo kwa siri.


Kwa sasa familia hizo zimegundua mbinu mpya ya kuwatahiri watoto wa kike wakiwa wadogo sana, kuepuka kukamatwa.


Ngariba wanaotumika kukeketa watoto, mara nyingi ni akina mama vikongwe wasiokuwa na ujuzi, taaluma za afya na hutumia vifaa butu, ambazo husababisha uvujaji mwingi wa damu na kuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa mengine.

No comments

Powered by Blogger.