WASANII KUTEKETEA KWA KUBWIA MADAWA YA KULEVYA, JE NINI TATIZO? TUPATIE MAONI YAKO
NI mtihani.
Ndivyo unaweza kusema, hasa baada ya kundi kubwa la vijana wenye umri
wa miaka 15 hadi 30 kujikuta likiteketea kutokana na matumizi ya dawa za
kulevya.
Kutokana
na hali hiyo, kundi la wasanii wa muziki wa kizazi kipya na vijana wa
kimaskini wamekuwa ni waathirika wakubwa hali inayotishia nguvu kazi ya
Taifa.
Kundi
la hilo la wasanii sasa limegeuka mateka, huku hali hiyo ikichangiwa na
wafanyabiashara wakubwa nchini, ambao wamekuwa wakiwashawishi kwa fedha
na hata kuwahonga magari ili waweze kutumia mihadarati.
MTANZANIA
ilizungumza na baadhi ya wasanii ambao sasa wamejikuta katika matumizi
ya mihadarati hiyo na hata kuonekana kuwaumiza huku wengine wakiwa kama
wendawazimu.
Mmoja
wa wasanii wa muziki wa kizazi kipya, Abubakari Katwila, maarufu
Q-Chief, ambaye anatajwa katika matumizi ya dawa za kulevya, alisema kwa
sasa ameacha baada ya kukubali kuwa alipotea.
Alisema wakati anaingia katika matumizi hayo ya mihadarati hakushawishiwa na mtu, bali alijikuta ametumbukia katika hali hiyo.
“Nilikuwa
muathirika wa dawa za kulevya, nimejitambua nimeacha mimi mwenyewe bila
kulazimishwa na mtu, huwezi kumtibu mtu ambaye hajajikubali hili ni
tatizo,” alisema.
FEROOZ
Ferooz
Mrisho ambaye katika miaka ya 2000 alitamba na wimbo wa Starehe ambao
ulikuwa ukihamasisha mapambano dhidi ya Ukimwi, ambaye kwa sasa
ameathirika na dawa hizo, alisema inamuwia vigumu kuachana na matumizi
ya dawa hizo.
Alisema
pamoja na hali hiyo, amejikuta akitenga bajeti kubwa ya fedha kwa
matumizi ya kutumia dawa, ingawa alipoulizwa ni wapi anaponunua hakuwa
tayari kutaja.
“Ninawaomba
wasanii wenzangu wasitumie dawa maana ni vigumu kuacha. Natamani sana
kurudi kama zamani ili heshima yangu iwepo ila inanisumbua, lakini
naamini iko siku,” alisema Ferooz.
Wasanii
wengine ambao wanahusishwa na tuhuma za matumizi ya dawa za kulevya ni
pamoja na Geez Mabovu, Daz Baba, T.I.D, Ray C, Lord Eyez, Rashidi
Makwilo ‘Chid Benz’, 20%, Terry Fanani, Sister P, Msafiri Diouf,
Rachael Kiuno, Mandojo, Domokaya, Rose Mhando na Nando ambaye hivi
karibuni alishiriki mashindano ya Big Brother (BBA).
Mmoja
wa wasanii hao ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazeti, alisema
kuwa pamoja naye kujikuta anatumia dawa za kulevya, lakini bado Serikali
inajua watu wanaoingiza dawa hizo na wameshindwa kuwachukulia hatua.
“Kula
dawa inahitaji gharama, maana inafika mahali ili niweze kupata kete
walau moja kila siku asubuhi inanibidi nitafute Sh 3,000. Lakini pia
hufika mahali natumia hadi Sh 15,000 kwa siku.
“Wapi
napata pesa? Unajua licha ya hii kazi yangu ila bado kuna jamaa zangu
wanene (wafanyabiashara) ambao nao hutumia, ukiwapigia simu hukosi
20,000 au hata 100,000. Na mimi nilipoingia katika matumizi haya jamaa
yangu mmoja alinishawishi kuwa nikitumia hii atanipa safari, kumbe
nilikuwa naonja ili kujua ubora, basi hadi leo nimejikuta natumia,”
alisema msanii huyo.
Matumizi
ya dawa za kulevya yanatajwa kusababisha vifo vya wasanii kadhaa
wakiwamo Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’, Aisha Mohamed ‘Aisha Madinda’,
Albert Mangwea ‘Ngwea’, Langa, Grace Mbawala na Esther Bondia.
Licha
ya hilo, taarifa za ndani zinaeleza kuwa aliyekuwa msanii nyota wa
Bongo Movie, marehemu Steven Kanumba pia anahusishwa na matumizi ya dawa
hizo.
Inalezwa
kuwa baada ya kifo chake, alikutwa katika kucha akiwa na chembe za unga
unaosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya, ambazo baada ya kutumia alikunywa
pombe kabla ya kuingia katika ugomvi unaodaiwa kusababisha mauti yake.
VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA
Kwa
mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya,
vita dhidi ya matumizi ya dawa hizo imeendelea kupata changamoto nyingi
kutokana na kukithiri kwa uingizaji wake.
Tume
hiyo ilidai kuwa kiwango cha dawa zinazoingia na kukamatwa kimepanda
kutoka kilo tatu za dawa aina ya Heroin mwaka 2008 hadi kilo 265.54
mwaka 2011 na kilo nne za dawa aina ya cocaine hadi kufikia kilo 128.30
kwa mwaka huo.
MSAKO WA WASANII WABWIA UNGA
Akizungumza
na MTANZANIA, Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Mihayo
Msikhela, alisema hivi sasa wapo kwenye msako dhidi ya wasanii ambao
wamekuwa wakisambaza ujumbe wa matumizi ya mihadarati hiyo.
Alisema wasanii hao ambao ndio kioo cha jamii, sasa wamekuwa wa kwanza katika kusambaza ujumbe wa matumizi hayo.
“Mimi
binafsi simfahamu Chid Benz kama ni mtu maarufu aliyekuwa akifahamika
kwa kiasi hicho, lakini baada ya kumuona kwenye mitandao ya kijamii
ndipo nikaanza kumfuatilia,” alisema Kamishna Msikhela.
Alisema endapo wakipata taarifa ya kwamba wanatumia hadharani na kuwakamata, basi watachukuliwa hatua kama wahalifu wengine.
“Hawa
wasanii tunawasaka nao watuhumiwe kama wahalifu wengine na
wakichukuliwa hatua itakuwa fundisho kubwa kwa vijana ambao walikuwa na
nia ya kujiingiza katika mtandao huo,’’ alisema.
Alisema
ni vema kwa vijana wasiwafuate watu maarufu ambao kwa namna moja ama
nyingine wanaushawishi mkubwa kiasi katika matumizi ya dawa hizo.
Kamishna
Msikhela alisema wimbi kubwa la vijana wenye umri kati ya miaka 15 na
30 ndilo ambalo linajiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya jambo
ambalo ni hatari kwa Taifa.
“Vijana
hawa ndio ambao wangekuwa tegemeo, vijana wa umri huo ndio ambao
wangekuja kuwa viongozi wa baadaye, yaani kwa umri huo ndiyo
wanaandaliwa kuwa madereva, mawaziri, wakulima, lakini leo wanakuwa
mateja, ni jambo la hatari sana,’’ alisema.
MIKAKATI
Kamishna
Msikhela alisema Jeshi la Polisi kwa sasa liko katika mkakati maalumu
wa kuhakikisha elimu katika jamii inatolewa ili wananchi waweze
kuelimika.
Alisema
ulimaji wa bangi mashambani ni mkubwa kuliko mirungi, lakini aliongeza
kuwa kama mateja mitaani wanapungua basi hata uingizaji wa dawa hizo kwa
sasa nao umepungua.
KAULI YA WAZIRI
Juzi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alisema wimbi la
magenge, wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya wameongezeka kwa
kasi.
Kutokana
na hali hiyo, alisema kuwa kwa wale wanaojihusisha kwa namna yoyote ile
ni vyema wakaamua kuachana nayo kabla hawajakumbwa na mkono wa dola.
Alitoa
kauli hiyo baada ya kufanya mazungumzo na mama mzazi wa msanii Chid
Benz, ambaye amepatwa na tatizo la matumizi ya dawa za kulevya.
“Inasikitisha
na haivumiliki kuona nguvu kazi ya Taifa inapotea huku wauzaji
wakinufaika kwa pesa haramu, ifahamike wazi vita ya Serikali dhidi ya
wauzaji ni kubwa kuliko wanavyofikiria,” alisema.
VIONGOZI WA DINI
Wakizungumza na MTANZANIA, viongozi mbalimbali wa dini walisema kuwa ipo haja kwa jamii na Serikali kuwa na hofu ya Mungu.
Askofu
Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Bukoba, Dk. Method Kilaini,
alisema kama viongozi wa dini inabidi watoe elimu ya dini kwa nguvu zote
na kuwaweka vijana wawe na hofu ya Mungu.
“Elimu
ya kumweka kijana katika maombi awe karibu na Mungu hili litasaidia
sana kujitoa katika mtego huo wa shetani na si vinginevyo,” alisema
Askofu Kilaini.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Hamis Mataka, alisema Serikali
haitakiwi kumwacha mtumiaji wa kawaida kwani naye ni muhalifu pia.
Alisema
vita hivyo ni vema vikafanyika kwa kuangalia kila eneo badala ya sasa
kupambana na waingizaji, huku watumiaji wakiachwa kwani suala hilo
haliwezi kumalizika.
“Kwa
upande wa dini tunatakiwa kuanza kuwaelimisha watoto wetu juu ya dhambi
hii huko kwenye madrasa sio kufundisha Kuran tu, wazazi sasa hivi
wanalea kidigitali, hivyo mtoto kufanya dhambi anaona ni kitu cha
kawaida.
“Tuanze
kuwaonyesha watoto wetu namna ya kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, hii naona
itapunguza, pili hata hao vijana walioathrika wasipelekwe tu ‘Sober
House’ kwa sababu ya matibabu, pia wapate nasaha kutoka kwa viongozi wa
dini ili wakibadilika wabadilike kiuhakika,’’ alisema Sheikh Mataka.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Maadili inayoshirikisha viongozi wa dini, Askofu William
Mwamlanga, alisema Taifa linahitaji maombi mazito kwani Serikali
imeshindwa kudhibiti hali hiyo na vijana wanaendelea kuangamia.
“Pia
kesho (leo) tuna kikao cha wajumbe wa dini zote ambao mimi ni
mwenyekiti wao, tutajadili hali hii kwani tulikubaliana sekta za dini
zisiwe chaka la kubebea dawa hizo haramu ambazo pia ni katazo la Mungu,”
alisema Askofu Mwamalanga.
VIONGOZI WA WASANII
Akizungumzia
hali hiyo, Rais wa Shirikisho la Wasanii wa Filamu Tanzania (TAFF),
Simon Mwakifamba, alisema dawa za kulevya ni janga la Taifa.
Alisema
ni vyema kila mmoja anapoona mwenzake ameathirika afikirie kwa makini
kuwa na yeye kesho anaweza kufika hapo alipo mwenzie.
Rais
wa Shirikisho la Madansa, Super Nyamwela, alisema baada ya kifo cha
wasanii wenzao, akiwamo Aisha Madinda, walichukua tahadhari kubwa
ikiwamo kufanya utafiti na kubaini kuwa wengi waliotumbukia katika
matumizi hayo walitumia sigara wakiwa kazini.
WALIONASULIWA WAKAKWAMA
Mara
kadhaa viongozi wa kitaifa wamekuwa wakichukua juhudi mbalimbali
ikiwamo kuwasaidia wasanii hao, akiwamo mwanamuziki Rehema Chalamila
‘Ray C’ ambaye alisaidiwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya
Kikwete kwa kuhakikisha analipia matibabu yake ili aweze kuachana na
dawa za kulevya.
Mbali
na huyo pia Chid Benz alisaidiwa na Meneja wa Dimond, Babu Tale kwa
kumpelea Sober House mjini Bagamoyo ambako alifanikiwa kuacha na baada
ya muda alirudia tena kutumia mihadarati hiyo.
Source: Mtanzania
No comments