Polisi Watinga Nyumbani kwa Gwajima....Mwenyewe Agoma Kufungua Mlango
Jeshi
la Polisi kwa mara nyingine jana lilizingira nyumba ya Askofu wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kwa kile lilichodai kuwa lilifika
kufanya uangalizi.
Taarifa ambazo zimethibitishwa na Askofu Gwajima mwenyewe, zinaeleza kuwa polisi walifika nyumbani kwake wakiwa katika gari lao.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, polisi hao walipojaribu kutaka kuingia nyumbani
kwa askofu huyo, walizuiwa mlangoni kwa sababu hawakuwa na kibali
chochote wala maelezo yanayojitosheleza ya kutaka kukutana na kiongozi
huyo wa kiroho.
Askofu Gwajima jana alikiri polisi hao kumfuata nyumbani kwake na hivyo kulazimika kumtafuta wakili wake mara moja.
“Ni
kweli walikuja wakiwa na gari la polisi, lakini walipofika nami
nilimpigia mwanasheria wangu ambaye aliniambia tuwaulize wametumwa na
nani na kama wana ‘search warrant’ (kibali cha kufanya upekuzi) au
‘arrest warrant’ (kibali cha kukamata),” alisema.
Askofu Gwajima alisema walipowauliza, walimtaja Afande Kingai kama ndiye mtu aliyewatuma, lakini hawakuwa na kibali chochote.
Kwa
mujibu wa Askofu Gwajima, mwanasheria wake alifanya mawasiliano ya simu
na Afande Kingai ambaye amepewa jukumu la kuwafuatilia wale wote
waliotuhumiwa katika sakata la dawa za kulevya na kumuuliza sababu za
kumfuata nyumbani.
“Afande
Kingai amemweleza mwanasheria wangu kuwa walikuwa wamekuja kwa ajili ya
‘observation’ (uangalizi) tu, kwa hiyo mwanasheria wangu akasema kama
ni ‘observation’ tu tusiwaruhusu kuingia ndani kwa sababu sheria ya
hivyo hakuna, na sisi tumewazuia hawakuingia ndani,” alisema Askofu Gwajima.
Alipoulizwa
kama kufuatwa kwake sasa na polisi kuna uhusiano wowote na kauli
alizozitoa kanisani kwake hivi karibuni kuhusu elimu ya Paul Makonda
ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Askofu Gwajima alisema huenda
ikawa hivyo, lakini akasisitiza kuwa hana uhakika kwa sababu
hajazungumza na askari waliomfuata.
Na
alipoulizwa kama anadhani ujio huo pia unatokana na andiko ambalo
linasambaa kwenye mitandao ya kijamii ambalo linasema Jumapili ijayo
mwalimu aliyemfundisha mtu mmoja anayetajwa kwa jina la Bashite
atakuwapo kanisani kutoa ushuhuda, Askofu Gwajima alikana akisema andiko
hilo si lake.
Pamoja na hayo, Askofu Gwajima alikwenda mbali na kuhoji: “Hata
kama ni kweli, sasa unaogopa mwalimu kuja… kanisani kwangu wapo watu
wengi waliosoma naye Bashite kuanzia shule ya msingi na Sekondari ya
Pamba… vyeti kama huna huna tu.”
Alipoulizwa
haoni kauli yake kwamba Rais Magufuli ni tofauti kabisa na Makonda
ilikuwa na nia ya kuwatenganisha viongozi hao, Askofu Gwajima alisema
aliyemtaja kwa kumshambulia ni Makonda na si Rais.
“Aliyenitaja
kwa kunishambulia katika sakata la dawa za kulevya ni Makonda na si
Rais, mimi nimemuongelea Makonda, mimi ni mtumishi wa Mungu siwezi
kuongozwa kwa ‘speculation’, si unajua hata Yesu alisema kama wewe huna
dhambi basi uwe wa kwanza kushika jiwe,” alisema Askofu Gwajima.
Alipoelezwa kuwa katika mahubiri yake ni kama anaonekana kumshtaki Makonda, askofu huyo alisema:
“Nilisema nitamshtaki kwa mahakama iliyo juu yake na nilisema Makonda
aombe radhi, angekuwa mstaarabu baada ya sakata lile yeye mwenyewe
angenipigia simu na kuniambia Gwajima nilikengeuka, lakini hajafanya
hivyo.”
Pamoja na hayo, Askofu Gwajima alisema kwa aliyoyafanya Makonda tayari amekwishamsamehe na ndiyo maana hajampeleka mahakamani.
No comments