Magufuli: Serikali haitatoa chakula cha bure kwa wenye njaa
Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
ameendelea kusisitiza kuwa kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada
kwa watakaopatwa na njaa ilihali wanaweza kuzalisha chakula katika
maeneo yao.
Rais Magufuli
ametoa kauli hiyo leo katika ziara yake mkoani Pwani, wakati
akizungumza na wananchi wa Somanga, Nangurukuru na Mchinga Moja, ikiwa
ni ziara yake katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.
Amepokea kero za wananchi katika maeneo hayo nakuwataka kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya chakula cha kutosha
"Najua
mmezoea kusikia maneno mazuri mazuri kuwa hakuna atakayekufa kwa njaa,
sasa mimi nasema usipofanya kazi, usipolima mazao na kupata chakula
wakati mvua inanyesha Serikali haitatoa chakula cha bure kwa wenye njaa,
ni lazima tufanye kazi, sasa hivi mvua zinanyesha limeni mazao ya
chakula" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli
amezungumza na wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero zao ambapo
amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo kuhakikisha mradi wa maji
uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya Shilingi
Bilioni 5, unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa Mwezi huu na pia
amepiga marufuku utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo wa
mazao.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli
amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Lindi kushughulikia migogoro ya wakulima
na wafugaji iliyoanza kuibuka mkoani humo na ameahidi kutoa Shilingi
Milioni 20 kusaidia ujenzi wa Zahanati ya Somanga.
Mbali na hayo Rais Magufuli
amewaagiza Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kujenga kituo cha
mabasi cha Nangurukuru na pia amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi
kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mhe. Hamidu Bobali
kuhakikisha anapeleka Daktari katika kijiji cha Mchinga Moja ili kutatua
kero ya wananchi kukosa huduma ya matibabu.
Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake kesho tarehe 03 Machi, 2017 hapa Mkoani Lindi
No comments